Mama Taifa Rachel Ruto, ametoa wiro wa ushirikiano dhabiti wa kimataifa katika kukabiliana na ghasia za kijinsia, dhuluma dhidi ya wanawake, ulanguzi wa binadamu na ongezeko la kudhulumiwa kwa watoto mtandaoni.
Alisisitiza mbinu jumuishi inayoleta pamoja serikali, jamii, sekta za elimu, afya,haki, taasisi za kidini, waajiri na taasisi za kilimo, katika kushughulikia dhuluma hizo.
Akizungumza kwenye mkutano wa pamoja wa Kenya na Romania kuhusu ghasia dhidi ya wanawake, ulanguzi wa binadamu na usalama wa watoto mtandaoni, ulioandaliwa Jijini Nairobi, Mama Rachel alisema ushirikiano wa Kenya na Romania, unatoa fursa kwa mataifa hayo mawili kujifunza kutoka kwa kila moja, na kubuni mazingira mwafaka ya kuimarisha uhusiano wa pamoja.
“Tungekabiliana na changamoto hizi kila taifa peke yake, lakini tumeazimia kuchukua njia ya pamoja ambayo ni ya kijasiri,” alisema Mama Taifa.
Aidha, alielezea wasiwasi kuhusu ongezeko la visa vya ulanguzi wa binadamu, akitoa wito wa juhudi za pamoja kuzuia, kuokoa, kuwarejesha nyumbani waathiriwa na kufunguliwa mashtaka wahusika wa vitendo hivyo.
Alisema Kenya imepiga hatua kubwa kukabiliana na ghasia za kijinsia, kwa kuwezesha swala hilo kuangaziwa katika ngazi za kitaifa.
Matamshi yake yaliungwa mkono na balozi wa Romania hapa nchini Gentiana Șerbu, aliyesema Romania imejitolea kuimarisha ushirikiano wake na Kenya.