Mchungaji maarufu wa kike nchini Tanzania Rose Shaboka ameibua mjadala mkali mitandaoni kufuatia semi zake wakati akihojiwa.
Katika mahojiano hayo, Rose ambaye anaripotiwa kuzozana na mumewe Mchungaji Nick Shaboka, alisema kwamba hawezi kusoma sana kiasi cha kupata digrii nne kisha aishie kuwa mke nyumbani.
“Yule mzee Mushi kule kijijini amenisomesha, kuanzia chekechea hadi Form Six, nikaenda Chuo Kikuu, nikapata Degree ya kwanza, ya pili, ya tatu, ya nne, nije kuishia kufua boksa, niishie tu kupika? Nooo!…” alisema mhubiri huyo.
Alishauri wanawake kufikiria kujijenga binafsi hata wanapokuwa ndani ya ndoa akisema, “Mwanaume anaheshimu mwanamke ambaye ana maisha nje ya mahusiano; mwanaume anaheshimu mwanamke ambaye anaweza kusimama bila yeye.”
Kauli hizo zimeibua mjadala kuhusu nafasi ya mwanamke katika kujenga taaluma, kujitegemea na namna ya kusawazisha maisha binafsi na majukumu ya familia.
Wengi wa wanaotumia mitandao nchini Tanzania wanahisi kwamba anapotosha wanawake wengi kwa kauli zake, wengine wakitoa maoni kwamba masomo hayafai kubadili mwanamke katika jamii.
Maoni mengine ni kwamba mwanamke kufanya majukumu yake katika ndoa sio kumdunisha hata ingawa ana kiwango cha juu cha masomo.
Huku haya yakijiri, kumekuwa na ripoti kwenye mitandao ya kijamii kwamba Rose na mume wake Nick Shaboka ambao wote ni wahubiri wanapitia kipindi kigumu katika ndoa yao.