Maafisa wa polisi wamefunga eneo la kuuzia pombe haramu katika mto Likii, kaunti ya Laikipia kwenye operesheni inayoendelea ya kukabiliana na pombe haramu.
Operesheni hiyo iliyotekelezwa na maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Nanyuki, ilisababisha kunaswa pia kwa vifaa vya utenegenezaji pombe zinazojumuisha tanki 6 za lita 100 kila moja na jiko sita, miongoni mwa zingine.
Polisi hao walipata lita 2,520 ya pombe haramu aina ya Kangara, na pombe nyingine iliyopakiwa kwenye mitungi mitano ya lita 20 kila moja.
Maafisa hao walimwaga pombe hiyo.
Huduma ya Taifa ya Polisi imesema operesheni hiyo ni sehemu ya juhudi za kusambaratisha utengenezaji na usambazaji wa pombe haramu, ambayo ni hatari kwa matumizi ya binadamu.
“Uchunguzi unaendelea kuwatambua na kuwakamata wanaohusika na utenegenezaji wa pombe haramu,” ilisema huduma hiyo ya polisi.