Aliyekuwa Waziri wa maswala ya Jinsia Aisha Jumwa, amejiunga na chama cha Wiper Patriotic Front, siku kadhaa baada ya kukigura chama cha United Democratic Alliance (UDA).
Jumwa alitangaza hayo leo Ijumaa baada ya kuwa mwenyeji wa kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, nyumbani kwake Kakuyuni, Malindi kaunti ya Kilifi.
Kulingana na mbunge huyo wa zamani wa Malindi, hatua yake ya kuondoka UDA, ilichochewa na kile alichotaja kupuuzwa kwa maslahi ya wakazi wa Kilifi.
Alifichua kwamba juhudi zimetekelezwa za kumnyamazisha kwa kubadilishana na zawadi za kisiasa, lakini alichagua kusimama kidete na kuwaunga mkono watu wa Kilifi.
Jumwa pia aliwahi kuhudumu wadhifa wa mwenyekiti wa Bodi ya Barabara nchini Kenya (KRB) kabla ya muhula wake kupigwa breki na mahakama.
Wakati huo huo Jumwa amemuidhinisha Kalonzo Musyka kuwania Urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, akielezea matumaini kwamba jamii ya Pwani itaunga mkono upande wa upinzani.
Akimkaribisha kwenye chama cha Wiper, kinara wa chama hicho Kalozno Musyoka alisema Wiper itamuunga mkono Jumwa, kuwania wadhifa wa Gavana wa Kilifi kwa tiketi ya chama hicho.
Kalonzo alisema chama cha Wiper kinajiimarisha kuwa nyumbani kwa watu wa Pwani, huku akiahidi kueneza umaarufu wake katika sehemu zote za nchi.
Aliwakumbusha wakazi wa pwani safari ya muda mrefu ya kisiasa aliyotembea na hayati Raila Odinga katika eneo la Pwani, kwenye mapambano ya kutafuta demokrasia na haki ya kijamii.
Chama cha Wiper pia kiliwazindua wagombeaji wake wa viti vya Ugavana katika eneo la Pwani ambao ni Mohamed Ali (Mombasa), Danson Mwashako (Taita Taveta), Aisha Jumwa (Kilifi) na Abdalla Shakilla (Lamu).