Msako dhidi ya mbolea ghushi waendelea

Magunia 3,500 ya aina mbalimbali za mbolea inayoshukiwa kuwa bandia, yalipatikana katika Kaunti ya Uasin Gishu

Marion Bosire
2 Min Read

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI imeongeza juhudi katika mapambano dhidi ya mtandao unaoshukiwa kusambaza mbolea bandia.

Hii ni baada ya kuwakamata washukiwa watatu zaidi na takriban magunia 3,500 ya aina mbalimbali za mbolea inayoshukiwa kuwa bandia katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Maafisa wa operesheni maalum katika DCI, wakiongozwa na taarifa za kijasusi, walivamia eneo la Kabenes, Kaunti Ndogo ya Soy, ambako waliwakamata Rose Chemeli, Vincent Kibet na Elias Kipkoech.

Mamlaka zilisema washukiwa hao bado wanazuiliwa wakisubiri kufikishwa mahakamani, huku mbolea iliyokamatwa ikihifadhiwa kama ushahidi.

Operesheni hiyo ya hivi punde imefanyika saa chache baada ya maafisa hao kukamata washukiwa wawili na magunia 624 ya mbolea inayoshukiwa kuwa bandia katika msako mwingine uliofanyika Kijiji cha Kapsubere, Karuna Hills, Kaunti Ndogo ya Moiben.

Joshua Ngetich na Lameck Odhiambo walikamatwa, huku washukiwa wengine wanne wakitorokea shamba la mahindi lililokuwa karibu na bado wanatafutwa.

Wapelelezi pia walipekua ghala lililoko Ziwa Sirikwa linalohusishwa na mshukiwa anayesakwa, Elphas Bett na kukamata magunia mengine ya mbolea yenye chapa za Elgon Kenya na Mavuno.

DCI inaamini mbolea hiyo imechanganywa isivyo halali au kuelekezwa kinyume cha sheria kutoka kwa mpango wa mbolea ya ruzuku ya serikali.

DCI imesema uchunguzi unaendelea huku mamlaka zikizidi kuwasaka wahusika wa mitandao ya uhalifu inayohatarisha maisha ya wakulima na usalama wa chakula nchini.

Share This Article