Ni afueni huku wafanyakazi wa viwanja vya ndege wakisitisha mgomo

Wafanyakazi wote wametakiwa kurejea kazini huku usafiri wa ndege ndani na nje ya Kenya ukitarajiwa kurejelewa.

Dismas Otuke
1 Min Read

Wafanyakazi wa viwanja vya ndege nchini wamesitisha mgomo ambao umedumu kwa takriban mwezi mmoja baada ya kutia saini makubaliano ya kurejea kazini Jumatatu usiku.

Chama cha wafanyakazi hao, KAWU, kimesitisha mgomo huo baada ya kuafikiana na Mamlaka  ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini, KAA, KCAA na kampuni ya ndege ya Jambojet.

KAWU imesema kuwa itaanza mazungumzo mara moja kuhusu nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi.

Mgomo huo ulisitisha  shughuli zote katika viwanja vya ndege nchini Kenya, huku wasafiri wakikwama katika uwanja mkubwa wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA wakati pia ndege zikilazimika kufutilia mbali safari zote.

Wafanyakazi wote wametakiwa kurejea kazini huku usafiri ndege ndani na nje ya Kenya ukitarajiwa kurejelewa.

KAWU imekubaliana kuhusu matakwa kadhaa  na serikali ikiwemo kutoadhibiwa kwa wote waliohusika kwenye mgomo huo.

Makubaliano hayo yamepatikana kufuatia mazungumzo ya muda mrefu Jumatatu jioni kati ya maafisa wa KAWU, KCAA, KAA na Jambojet.

Nao uliafikiwa chini ya upatanishi wa Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi nchini (COTU) Francis Atwoli.

Share This Article