Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI, wamewatia nguvuni washukiwa watano wa ulanguzi wa dhahabu.
Watano hao wanaojumuisha afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya AFREX Bridge Connections Lamarca J. Benjamin almaarufu Morlon, Jean Emmanuel, Samson Kibet Sirkoi, Lucy Gitonga, Rose Kambua na Justine Adhiambo, walikamatwa kutoka sehemu tofauti za nchi.
Kupitia ukurasa wa X, idara ya DCI ilisema mlalamishi aliandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha uwanja wa ndege wa Wilson Januari 29, 2025, akisema aliarifiwa kuhusu mshukiwa mkuu Lamarca kwamba anauza kilo 550 za dhahabu.
Kulingana na mlalamishi huyo, dhahabuhiyo ilidaiwa kuhifadhiwa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, na ilitarajiwa kusafirishwa iwapo malipo ya dola 120,000 zitatolewa.
DCI ilisema mlalamishi huyo alitoa malipo hayo lakini mchezo wa paka na panya kati yake na washukiwa hao ukaanza.
Maafisa hao walianzisha uchunguzi na kuvamia kampuni ya AFREX Bridge Connections ambapo walipata ushahidi muhimu na kuwatia nguvuni washukiwa wawili Lucy Gitonga na Rose Kambua.
Mnamo Januari 31, 2024 mshukiwa Samson Kibet Sirkoi pia alitiwa nguvuni kabla ya maafisa hao kufululiza katika mtaa wa Mount Kenya Wildlife katika hifadhi ya Ol Pejeta eneo la Nanyuki mnamo Februari 2, 2024 na kumkamata Lamarca almaarufu Morlon na Justine Adhiambo. Washukiwa hao walipatikana na bastola aina ya Glock, risasi 96, pingu za polisi, tarakilishi na leseni 6 za uchimbaji madini amabazo muda wa kutumika umekamilika.

Washukiwa hao waliwapeleka maafisa wa polisi katika makazi yaliyoko mtaani kileleshwa ambapo ushahidi zaidi ulipatikana, zikiwemo guruneti 14, vazi la kuzuia risasi na stampu za kampuni.
DCI ilisema kuwa washukiwa wawili Lucy na Kambua walifikishwa mahakamani huku wachunguzi wakikubaliwa kuwazuilia huku uchunguzi ukiendelea.
Washukiwa hao wengine walitarajiwa kufikishwa mahakamani Februari 4, 2025.