Mtu mmoja amefariki na wengine zaidi ya 12 kujeruhiwa baada ya gari kuendeshwa kuelekea kwa watu waliokuwa kwenye gwaride la LGBTQ mjini Berlin, nchini Ujerumani kulingana na polisi.
Tukio hilo lililotokea Jumamosi saa 4 usiku kwa saa za eneo hilo na kusababisha polisi kusitisha hafla hiyo saa chache baada ya kuanza.
Kulingana na uchunguzi wa mwanzo wa polisi, gari jeupe liliwagonga watu kadhaa katika Bustani ya Tiergarten katikati ya jiji, karibu na njia ya maandamano ya Pride, kabla ya kugonga mti, msemaji wa polisi Florian Nath alisema.
Katika chapisho kwenye X, polisi walisema angalau watu 16 walijeruhiwa na baadhi yao walikuwa katika hali mahututi. Walitoa wito kwa watu wote kuondoka mara moja katika eneo la tukio.
Picha iliyotolewa na polisi wa Berlin tarehe 26 Julai 2026 ilionyesha mshukiwa wa umri wa miaka 21 katika ombi la umma la kusaidia kumkamata.
Polisi waliongeza kuwa gari husika lilitelekezwa katika eneo la tukio ndani ya bustani hiyo—eneo lenye miti ambapo gwaride hilo huishia—na kwamba walikuwa wanaendesha msako mkali wa kuwatafuta washukiwa.
Mapema Jumapili, polisi walisema walikuwa wamemtambua mshukiwa lakini bado hawajamkamata. Mshukiwa huyo ni mwanaume anayefahamika na mamlaka na anayedhaniwa kuwa na uhusiano na kile walichokiita “makundi ya Kiislamu” mjini Berlin, kulingana na Nath.
“Msako wetu wa kumtafuta mtu huyu unaendelea kwa kasi kubwa,” msemaji huyo alisema bila kutaja jina lake.