Idadi ya watu waliofariki kutokana na mlipuko mpya wa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imeongezeka hadi watu 80, kulingana na Kituo cha Afrika cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa (Africa CDC).
Awali kituo hicho kilikuwa kimeripoti vifo 65 na maambukizi 245 katika wilaya ya Ituri Mashariki mwa DRC, huku maeneo yaliyoathiriwa pakubwa yakiwa ni Mongwalu na Rwampara maarufu kwa uchimbaji madini ya dhahabu.
Afrika CDC ilisema itashiriki meza ya mazungumzo na Uganda na Sudan Kusini ambao ni majirani wa DRC, kwa lengo la kuzuia msambao wa ugonjwa huo na kuimarisha uchunguzi wa mipakani.
Hadi kufikia sasa hakuna tiba iliyothibitishwa kutibu ugonjwa wa Ebola, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likisema asilimia 50 ya watu ambao huambukizwa ugonjwa huo hufariki.