Mwanamume ahukumiwa maisha gerezani kwa dhuluma za kimapenzi

Tom Mathinji
1 Min Read
Mwanamume ahukumiwa maisha gerezani kwa kudhuluma za kimapenzi.
Mahakama moja ya Eldoret imemhukumu mwanamume kifungo cha maisha gerezani kwa kumdhulumu kimapenzi msichana wa umri wa miaka 11.

Hakimu Mkuu Caroline Wattimah alitoa hukumu hiyo baada ya kumpata mshukiwa huyo na kosa hilo analodaiwa kutekeleza kati ya  Oktoba 21, 2024 na Novemba 10, 2024, katika eneo la Kamagut, kaunti ndogo ya Turbo, kaunti ya Uasin Gishu.

Wakati wa vikao vya kusikiliza kesi hiyo, mahakama ilifahamishwa kuwa mshukiwa ambaye alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mama ya msichana huyo, alimdhulumu kimapenzi msichana huyo nyumbani kwa mamake, huku akimtishia kuwa atamwadhibu iwapo atatoa habari hizo.

Huku ukiwasilisha ushahidi, upande wa mashitaka uliitaka mahakama hiyo kutoa adhabu kali zaidi kwa mshukiwa huyo ambayo ni kifungo cha maisha gerezani.

Wakati huo huo, upande wa mashtaka ulitoa wito kwa mahakama hiyo kumtangaza mshukiwa huyo kuwa hatari kwa makosa ya kimapenzi, na kwamba mwathiriwa apewe fursa ya kupata usaidizi wa kimatibabu ikiwa ni pamoja na ushauri nasaha.

TAGGED:
Share This Article