Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amefanya mabadiliko kwenye Afisi za Utawala wa Taifa kote nchini, huku akiwahamisha na kuwapandisha vyeo maafisa wa utawala.
Mabadiliko hayo yaliwalenga Warakibu wa maeneo na Makamishna wa Kaunti, huku yakinuia kuimarisha utoaji huduma na ushirikishi wa shughuli za serikali kote nchini.
Baadhi ya waliohamishwa ni pamoja na Mrakibu wa eneo la Pwani Rhoda Onyancha, ambaye amepelekwa kuhudumu katika eneo la Nairobi, huku Paul Rotich akihamishwa kutoka eneo la Mashariki na kupelekwa Pwani.
Mrakibu wa eneo la Magharibi Samson Macharia Irungu na mwenzake wa eneo la Nyanza Flora Nkatha Mworoah wamehamishiwa Makao Makuu katika afisi ya Rais.
Kamishna wa kaunti ya Meru Jacob Muganda amepandishwa cheo na kuwa Mrakibu wa eneo la Mashariki huku mwenzake wa Kakamega Onesmus Musyoki Kyatha akichukua hatamu ya Mrakibu mpya wa eneo la Nyanza.
Allan Machari, aliyekuwa akihudumu katika Makao Makuu kwenye Afisi ya Rais, sasa anachukua wadhifa wa mrakibu wa eneo la Magharibi mwa nchi.
Murkomen amesema uhamisho huo umetokana na uzoefu wa kikazi na utendakazi wa maafisa husika katika kushughulikia masuala ya usalama na malalamishi kuhusu utoaji huduma.
Mabadiliko hayo ya warakibu wa maeneo ambayo pia yameathiri makamishna 16 wa kaunti na manaibu kamishna 7 wa kaunti, yanaanza kutekelezwa mara moja.