Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, amepuzilia mbali uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu majukumu yake ya kiongozi wa chama cha Ford Kenya na Spika wa bunge, akisema uamuzi huo hauna msingi wa kisheria.
Kupitia mshauri wake wa maswala ya sheria Benson Milimo, Wetang’ula alibainisha kuwa Mahakama haikutoa maagizo yoyote kumtaka awache kushikilia moja ya afisi hizo.
“Ningependa kufahamisha taifa na chama cha Ford Kenya hakuna wasiwasi. Kile ambacho Mahakama ilifanya nikutoa maoni yake ambayo hayana madhara yoyote,” alisema Milimo kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.
Mshauri huyo aliendelea kusema, uamuzi huo wa mahakama haukumshurutisha Wetang’ula kuacha kushikilia wadhifa wa kiongozi wa chama cha Ford Kenya au spika wa bunge la taifa.
Hata hivyo, alithibitisha kuwa Wetang’ula na chama chake, watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa Mahakama Kuu nyadhifa za Wetang’ula.
“Hii inamaanisha kuwa Moses Masika Wetang’ula ataendelea kushikilia wadhifa wa kiongozi wa chama cha Ford Kenya na Spika wa bunge la taifa.
Majaji hao walimpata Wetang’ula na hatia ya ukiukaji wa katiba, wakidokeza kuwa angeondoka kuwa kiongozi wa chama alpotwikwa jukumu la kuwa Spika wa bunge.
“Hatua ya kushikilia nyadhifa mbili ni kinyume na katiba,” ilisema Mahakama Kuu.
“Punde tu alipochaguliwa kuwa Spika, alifaa kuondoka kama kiongozi wa chama cha Ford Kenya,” iliongeza Mahakama hiyo.