Viongozi wa EAC na SADC wakongamana Tanzania kutatua mzozo nchini DRC

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais Ruto awasili Tanzania kuhudhuria mkutano wa pamoja wa EAC na SADC kuhusu mzozo nchini DRC.

Rais William Ruto, amewasili nchini Tanzania, kuhudhuria mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),  kuhusu mzozo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki aliwaongoza viongozi wengine wakuu serikali kumuaga Rais Ruto katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

“Tumemuaga Rais William Ruto akielekea nchini Tanzania, kuhudhuria mkutano wa pamoja wa  EAC-SADC, kuhusu hali ilivyo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),” alisema Kindiki kupitia ukurasa wake wa X.

Rais Ruto aliitisha mkutano huo akiwa mwenyekiti wa EAC, ili viongozi hao watafute mbinu za kusitisha mapigano  Mashariki mwa DRC kati ya waasi wa M23 na jeshi la nchi hiyo.

Kulingana na Ruto Marais  Suluhu Samia Hassan wa Tanzania, Felix Tshisekedi wa DRC, Paul Kagame wa Rwanda, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Yoweri Museveni wa Uganda na  Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia, walithibitisha watahudhuria mkutano huo mjini Dar es Salaam, Tanzania.

Kongamano hilo la marais kuhusu mzozo huo  nchini Congo unatarajiwa kufanyika leo na unafuatia ule wa mawaziri wa kigeni wa mataifa hayo uliofanyika jana mjini Dar es Salaam, ambapo  Kenya iliwakilishwa na waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *