Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, ametoa wito kwa wakazi wa eneo la Magharibi mwa nchi, kushirikiana na kuunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais William wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuchanga fedha katika kaunti ya Vihiga iliyoandaliwa na mwakilishi mwanamke Beatrice Adagala, Mudavadi aliwahimiza viongozi kutoka eneo hilo kuungana na kuangazia mwelekeo sawa wa kisiasa.
“Eneo la Magharibi lazima liungane na kuzungumza kwa sauti moja. Tuna nguvu tunapotembea pamoja,” alisema Mudavadi.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi wa eneo la Magharibi, akiwemo Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula na mbunge wa Sirisia John Walukhe, huku eneo hilo likijiandaa kwa mkondo wa kisiasa utakaochukua kabla ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Spika Wetang’ula, aliunga mkono wito wa ushirikiano, akidokeza kuwa eneo hilo litanufaika pakubwa iwapo litazungumza kwa sauti moja kuhusu maswala ya maendeleo.
“Tumekuwa kwa siaka kwa muda mrefu, na tunafahamu kuwa katika siasa bila kujali kiwango cha hekima ulichonacho, bila kushirikiana na wengine utaambulia patupu. Kama wakazi wa eneo ili tunapaswa kushirikiana pamoja na kuzungumza kwa sauti moja katika maswala ya maendeleo huku tunapomuunga mkono Rais William Ruto,” alisema Wetang’ula.
Kwa upande wake, mbunge Walukhe alitetea hazina ya maendeleo ya maeneo bunge NG-CDF, akionya dhidi ya hatua zozote za kuvunjilia mbali hazina hiyo.
Alihoji kuwa hazina hiyo imeendelea kupiga jeki miradi ya maendeleo katika maeneo ya mashinani hususan katika elimu na miundomsingi.