Shughuli zasimama mashabiki wa Arsenal wakifunga barabara Nairobi

Ni mara ya kwanza kwa "The Gunners" kushinda ligi Kuu Uingereza baada ya miaka 22.

Dismas Otuke
1 Min Read

Mashabiki wa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Uingereza, Arsenal, siku ya Jumapili walifunga barabara za katikati ya jiji la Nairobi kusherehekea ushindi.

Mamia ya mashabiki hao, wengi wao wakivalia jezi za Arsenal, waliimba nyimbo huku wakipiga densi na kuwalazimu wenye magari kuyaegesha ili kutoa fursa kwa shamrashamra.

Wakiimba wimbo wa “We Are the Champions, yaani Sisi ni Mabingwa”, mashabiki hao waliokuwa wakifanya maandamano ya amani walisitisha shughuli katikati ya jiji.

Msafara huo ulianzia katika eneo la Ambassador, ambapo wengine walikuwa wakiuza jezi,Vuvuzela na mitandio yenye nembo ya Arsenal, walipokusanyika kabla ya kuanza kuzunguka.

Sherehe za ushindi wa Arsenal pia zimeshuhudia maeneo ya Ngong  Hills na Eldoret.

Mashabiki wengine walipiga foleni ndefu kuzuru kaburi la aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Hayati Raila Odinga katika eneo la Opoda Farm mapema Jumapili.

Arsenal watatawazwa mabingwa wa Ligi Kuu Uingereza Jumapili baada ya mechi ya kufunga msimu ugenini dhidi ya Crystal Palace.

Ni mara ya kwanza kwa “The Gunners” kushinda Ligi Kuu Uingereza baada ya miaka 22.

Share This Article