Huduma ya taifa ya polisi inapojizatiti kuboresha uhusiano wake na jamii kupitia mpango uliozinduliwa almaarufu Community Policing, maafisa wengi wa polisi wanatia bidii za mchwa kuhakikisha mpango huo unafanikiwa.
Kupitia mpango huo, maafisa wa usalama hushirikiana na wananchi kuhakikisha visa vya utovu wa usalama vinatokomezwa kupitia mfumo dhabiti wa upashanaji habari.
Ashimosi Shelvin, ni miongoni mwa maafisa wa huduma ya taifa ya polisi ambaye azma yake ni kuu ni kuweka tabasamu kwa wananchi kwa kuwahudumia bila ubaguzi.
Shelvin, anayesimamia kituo cha polisi cha Gachuba, Kaunti ya Nyamira, amelimbiliziwa sifa sufufu na wakazi wa eneo hilo, kutokana na huduma bora anazotoa bila kuchoka katika eneo hilo.
Kulingana na wakazi hao, afisa huyo wa kupigiwa mfano, hushughulikia malalamishi yote yanayowasilishwa katika kituo hicho kwa wakati, na kuleta furaha isiyo kifani katika nyoyo za wakazi hao.
“Tangu alipochukua uongozi katika kituo hicho cha polisi, utoaji huduma umeimarika huku kesi zikishughulikiwa kwa wakati,” alisema Pamela Mogaka mkazi wa Gachuba.
Raia wa eneo hilo wamesema wanajihisi salama zaidi chini ya afisa huyo, na wana imani kubwa na utenda kazi wake.
“Afisa Ashimosi anasikiliza malalamishi yetu bila upendeleo na kuhakikisha kila kesi inashughulikiwa kwa haki,” aliongeza Pamela Mogaka.
Kwa mujibu wa Mogaka, kunapotokea swala la dharura, afisa huyo huwakusanya maafisa wake haraka iwezekanavyo bila kupoteza hata punje la sekunde na kulishughulikia vilivyo.
Uadilifu na uwazi wake katika kushughulikia masuala ya kijamii yamechangia kuimarika kwa uhusiano kati ya polisi na wananchi, hali ambayo imesaidia kupunguza migogoro na kuongeza ushirikiano wa jamii na vyombo vya usalama.
Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, amekuwa katika mstari wa mbele kupigia debe utekelezwaji kikamilifu wa mpango wa community policing kama njia muhimu ya kuimarisha usalama hapa nchini.
“Community policing ni nguzo kuu katika kudumisha amani kote nchini,” alisema Kanja.
Shelvin, anaendelea kusifiwa kama mfano bora wa uongozi wa polisi unaoendeshwa kwa misingi ya haki, uadilifu, na huduma bora kwa wananchi.