Kindumbwendumbwe cha ubingwa wa ligi kuu ya Kenya katika soka kitaingia mechi za mzunguko wa 20 mwishoni mwa juma hili kwa mechi tisa, kilele kikiwa Tusker FC dhidi ya Police FC.
Mechi nne zimeratibiwa kuchezwa Jumamosi, huku nyingine tano siku ya Jumapili.
Bidco United watafungua ukurasa saa saba katika uwanja wa Machakos, dhidi ya Nairobi City Stars, kabla ya kuwapisha Sofapaka watakaozuru Bandari uwanja wa Mbaraki.
Mabingwa watetezi Gor Mahia, watawatembelea Mathare United ugani Dandora, mechi zote mbili zikipigwa pia saa tisa.
Tusker FC wanaoongoza jedwali watafunga ratiba saa kumi dhidi ya Police FC, walio katika nafasi ya pili katika uchanjaa wa Machakos saa kumi alasiri, timu zote zikiwa na alama sawa 37.
Siku ya Jumapili KCB watashuka uwanjani Machakos saa saba dhidi ya Murang’a Seal nao wanajeshi Ulinzi wakabiliane na Kakamega Homeboyz kiwarani Dandora pia saa saba.
Mara Sugar watawaalika Talanta FC saa nane katika uwanja wa Awendo Green, wakati Shabana FC wakiwa ziarani Machakos dhidi ya Posta Rangers saa kumi, huku AFC Leopards wakimenyana na Kariobangi Sharks.