Diplomasia itafanikisha upatikanaji amani DRC, asema Rais Ruto

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto.

Rais William Ruto, ametoa wito wa kusitshwa vita mara moja na kukumbatia juhudi za kidiplomasia, katika kutatua mzozo unaoshuhudiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akizungumza wakati wa Kongamano la pamoja la Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ile ya Kusini mwa Afrika (SADC) Jijini Dar es Salaam Tanzania, Ruto alihimiza pande zote katika mzozo huo, kushiriki mazungumzo na kuchukua hatua za pamoja katika kuleta uthabiti.

“Hali iliyozuka hivi karibuni ya uhasama katika eneo la Goma na viunga vyake, ni ukumbusho wa kuongezeka kwa hali tete na hatua za pamoja ndio njia ya pekee ya kuleta suluhu itakayokubalika,” alisema Rais Ruto.

Kiongozi wa taifa alizihimiza pande zinazozozana ikiwa ni pamoja na kundi la M23 na jeshi la ulinzi la DRC, kusitisha mapigamo mara moja.

“Tunashirikiana pamoja kuhimiza pande zote kukomesha mapigano, hususan kwa kundi la  M23 kusimamisha hatua ya kutwaa maeneo zaidi na  jeshi la DRC likome hatua za kujibu mashambulizi,” alisema Rais Ruto.

“Usalama wa DRC ni muhimu, sio tu kwa uthabiti wa taifa hilo, lakini pia kwa ukuaji na utangamano wa EAC na SADC. Tunatoa wito kwa pande zote kushiriki mazungumzo, ushirikiano na zaidi ya yote ulinzi wa maisha ya raia,” aliongeza Rais Ruto.

Ruto, ambaye pia  ni mwenyekiti mwenza wa mkutano huo, alipuuzilia mbali utumizi wa kijeshi katika kusuluhisha mzozo huo, akihimiza utumizi wa mbinu za kidiplomasia kukabiliana na chanzo za mzozo huo.

Wakati huohuo kiongozi wa taifa, aipendekeza kuunganishwa kwa michakato ya amani ya Luanda na ile ya Nairobi kuwa moja, ili kuepusha hatari ya kuwepo juhudi tofauti ambazo huenda zikahujumu juhudi za kutafuta amani.

Rais Ruto na mwenzake wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, ni wanaongoza kwa pamoja mkutano huo, huku Rais wa DRC  Félix Tshisekedi, akihudhuria kwa njia ya video.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *