Idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), imesema maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa wawili wa ugaidi Mandera, waliokuwa wakipanga kuwateka nyara raia wa kigeni wanaofanya kazi katika eneo hilo.
Kupitia ukurasa wake wa X, idara hiyo ilisema baada ya maafisa wa polisi kupokea habari za kijasusi, walimkamata mshukiwa mkuu Isaac Abdi Mohamed, almaarufu Kharan Abdi Hassan mwenye umri wa miaka 29.
Anadaiwa kuingia hapa nchini kutoka El-ade nchini Somalia na kughushi stakabadhi kadhaa kujisingizia kuwa raia wa Kenya.
“Baada ya uchunguzi wa kina, ilibainika kuwa mshukiwa huyo alitarajiwa kumlipa mshirika wake wa hapa nchini shilingi 100,000, ili awateke nyara, kabla yeye na mwenzake Noor Yacob Ali mwenye umri wa miaka 29 kuwasafirisha hadi El-ade kwa ada ya shilingi 300,000,” ilisema DCI.
Operesheni ingine ilitekelezwa na maafisa wa polisi Jumanne asubuhi na kusababisha kukamatwa kwa mshukiwa mwingine Yacob Ali, katika eneo la Metameta mjini Mandera.
Washukiwa hao wawili wanazuiliwa, huku wakihojiwa zaidi kabla ya kufunguliwa mashtaka ya kuwa wanachama wa kundi la kigaidi.