Maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kutoka Ruiru, wamemkamata Dennis Wafula Wanabisi, ambaye ni afisa wa DCI Kibwezi kwa kuhusika katika wizi wa kimabavu Julai 22,2024 eneo la Mtito Andei.
Kulingana na DCI kupitia ukurasa wake wa X, maafisa wa polisi walipokea ripoti kuhusu visa vya wizi katika kituo cha kibiashara cha Yikisaya, katika kaunti ndogo ya Kibwezi.
Walipowasili, maafisa hao waligundua kuwa majambazi hao walikuwa wamevalia sare za polisi na walikuwa na bastola. Walivamia klabu ya 021 na kuwaibia wateja na wahudumu jumla ya shilingi 50,000. Katika tukio hilo, mhudumu mmoja alipigwa risasi tumboni na kujeruhiwa vibaya.
Baadaye, majambazi hao walifululiza hadi kituo cha kibiashara cha Darajani, na kuingia kwa nguvu katika sehemu ya burudani ya Seton, walifyatua risasi hewani mara mbili na kuwaibia wahudumu na wateja jumla ya shilingi 25,850 pamoja na simu mbili za mkononi.
Uchunguzi wa awali ulimhusisha afisa Wanabisi na visa hivyo au ana habari muhimu kuhusu visa hivyo vya wizi. Maafisa wa polisi walitwaa bastola yake, huku maganda ya risasi yakipelekwa katika makao makuu ya DCI kwa uchunguzi wa maabara.
Matokeo ya uchunguzi huo yalibainisha kuwa, risasi zilizofyatuliwa zilitoka kwa bastola ya Wanabisi.
Alifikishwa katika mahakama ya Makindu jana Jumatatu, huku maafisa wa polisi wakiruhusiwa kumzuilia kwa siku 14 kuwawezesha kukamilisha uchunguzi.