Mshukiwa mkuu wa mauaji ya Tob Cohen, Sarah Wairimu, amepata pigo baada ya Mahakama Kuu kumyima dhamana.
Katika uamuzi wake leo Jumanne, Jaji Diana Kavedza amesema itakuwa si vyema kumwachilia mshukiwa kwa dhamana kabla ya mashahidi wawili wakuu katika kesi hiyo kutoa ushahidi wao.
“Ikiwa ataachiliwa kabla ya mashahidi wawili wakuu kutoa ushuhuda, huenda akaingilia kesi hiyo,” amesema Jaji Kavedza.
Jaji huyo ameagiza Wairimu kuendelea kuzuiliwa katika gereza la Langata hadi upande wa mashtaka uwalete mahakamani mashahidi hao watakaotoa ushahidi wao faraghani.
Wairimu anatuhumiwa kwa kumuua mumeme Tob Cohen miaka 6 iliyopita.
Mshukiwa huyo amekanusha mashtaka ya mauaji ya Cohen ambaye alikuwa mfanyabiashara kutoka nchini Uholanzi.
Taarifa hii imechangiwa na mwandishi wetu wa mahakamani Ruth Wambui