Jose Chameleone kufanyiwa upasuaji

Mwanamuziki huyo amekuwa nchini Marekani tangu mwezi Disemba kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa kongosho.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Jose Chameleone atafanyiwa upasuaji wakati wowote kutoka sasa nchini Marekani baada ya kuugua ghafla nyumbani.

Mwimbaji huyo alisafiri hadi Marekani mwezi Disemba mwaka jana kwa ajili ya matibabu ambapo alikaa hospitali kwa muda na kisha kuruhusiwa kwenda nyumbani ambapo amekuwa chini ya uangalizi.

Rafiki yake ambaye pia ni mwenyeji wake nchini Marekani Juliet Zawedde ndiye alitangaza kuugua kwa hivi punde kwa Chameleone na upasuaji anaotarajiwa kufanyiwa.

Alichapisha video inayoonyesha wahudumu wa dharura wakijiandaa kumbeba Chameleone anayeonekana mwenye maumivu makali kutoka kwenye kiti.

“Rafiki yangu hajihisi vizuri leo, amepelekwa hospitalini. Ninakuombea rafiki yangu, Chameleone ninajua kwa sasa hauko sawa.” aliandika Juliet chini ya video hiyo.

Aliendelea kumhakikishia kwamba anapendwa na kusaidiwa na wengi wakati huu.

Mwezi Disemba aliugua na kulazwa katika hospitali ya Nakasero jijini Kampala nchini Uganda, kufuatia kile kilichotajwa kuwa maumivu makali ya tumbo.

Uchunguzi wa kimatibabu ulibaini kwamba anaugua ugonjwa wa kongosho ambao mara nyingi hutokana na unywaji pombe kupita kiasi.

Madaktari wanaripotiwa kushauri kwamba apatiwe matibabu bora na ya haraka ili kuzuia matatizo zaidi.

Chameleone alilazwa katika hospitali ya Nakasero katika chumba cha wagonjwa mahututi na baada ya siku 11 madaktari wakashauri atafute matibabu bora nje ya nchi.

Gwiji huyo wa muziki na kakake wanaishi nyumbani kwa rafiki yake wa asili ya Uganda Juliet Zawedde ambaye ni mfanyabiashara.

Hata katika hali yake ya kiafya, Chameleone na Zawedde wameonekana kwenye picha na video wakifurahikia maisha nchini Marekani kiasi cha kusababisha uvumi kwamba huenda ni wapenzi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *