Kansiime na Skylanta waashiria utengano

Ujumbe wa Kansiime na wimbo wa Skylanta wa hivi punde zaidi vinaashiria utengano.

Marion Bosire
2 Min Read

Mchekeshaji wa Uganda ambaye pia ni mwigizaji Anne Kansiime na mume wake Skylanta wanaashiria kwamba wameachana.

Februari 16, 2025, Kansiime alichapisha ujumbe fulani kwenye Instagram ambao uliwafanya wengi wadhanie kwamba ameachana na mumewe huku Skylanta akitoa wimbo unaozungumzia mpenzi wa zamani.

“Siku moja mtu ambaye umejitolea sana kwake atabadilika na kusema kwamba yeye hakuitisha, na hilo litakuumiza kwa sababu ni ukweli.” aliandika Kansiime.

Aliendelea kuelezea kwamba siku hiyo ilifika kwa maisha yake na ni Februari 16, 2025 akiongeza kusema kwamba anasonga mbele kwani yeye ni “upendo na upendo lazima upendwe”.

Skylanta naye ametoa wimbo uitwao ‘Ex’ yaani mpenzi wa awali ambao unahadithia jinsi aliteswa na mpenzi wake wa zamani.

Wimbo huo ulizinduliwa yapata wiki moja iliyopita na unarejelea mpanzi huyo wa zamani kuwa mmiliki wa nyumba za kukodisha ambaye kamwe hana utu.

Unasema mpenzi huyo alikuwa na marafiki wanne wa karibu, simu yake haikuwa inalia akiwa nyumbani na aliteseka kimya kimya kwa muda kabla ya kuhadithia rafiki yake.

Skylanta kwenye huo wimbo anarejelea rafiki yake kwa jina Bruno ambaye alimshauri aachane na mwanamke huyo.

Wawili hao hata hivyo hawajajitokeza wazi wazi kutangaza kwamba wameachana.

Wamekuwa wapenzi kwa muda na Aprili 2021 walibarikiwa na mtoto wa kiume kwa jina Selassie Ataho. Mwezi Juni mwaka huo wa 2021, Skylanta alimvisha Kansiime pete ya uchumba.

Kansiime aliwahi kuwa kwenye ndoa nyingine awali kabla ya uhusiano wake na Skylanta.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *