Mchekeshaji Eric Omondi ameapa kumsaidia jamaa kwa jina Isindu ambaye aliwahi kuhudumu katika kundi lake kama meneja wa mipangilio na vifaa.
“Isindu alifanya kazi na kundi langu kama meneja wa mipangilio na vifaa kutoka mwaka 2011 na mwaka 2017.” aliandika Omondi.
Haya yanajiri baada ya video ya jamaa huyo kuchapishwa mitandaoni ambapo alionekana akiokota takataka kwenye majaa.
Omondi alichapisha video inayomwonyesha akimzuru Isindu kwenye makazi yake duni na kisha kumpeleka kwake kwa mazungumzo.
Kulingana na maelezo yake, Isindu ana matatizo ya kiakili yanayotokana na msongo wa mawazo na anahimiza kwamba afya ya akili ya wanaume itiliwe maanani sana humu nchini.
“Afya ya akili ya wanaume na msongo wa mawazo ni tatizo la ulimwengu mzima.Wanaume huteseka sana kimya kimya.” alisema Omondi katika chapisho lake akiongeza kwamba wanaume ndio viongozi wa familia na iwapo wanatakiwa kuongoza jamii, lazima hali hiyo izungumziwe la sivyo jamii nzima itakuwa na matatizo.
Mchekeshaji huyo anasema alikaa na Isindu kwa siku nzima na alishuhudia akikumbwa na matatizo mara tatu kutokana na hatua ya Omondi ya kumkataza asitumie dawa za kulevya, japo yeye mwenyewe hajakubali kwamba aba tatizo.
Hata hivyo Omondi ametoa hakikisho kwamba atafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba Isindu ambaye pia ni mwanamuziki anapata usaidizi anaostahili na kurejelea hali yake ya kawaida.
Matatizo yake yanadaiwa kutokana na kifo cha mamake mzazi na matatizo ya ndoa.