Jude Okoye aachiliwa baada ya miezi miwili kizuizini

Aliwekwa korokoroni baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana kwenye kesi ya utakatishaji wa fedha iliyowasilishwa dhidi yake na EFCC.

Marion Bosire
2 Min Read

Jude Okoye kaka mkubwa wa wanamuziki mapacha Peter na Paul Okoye wa kundi la muziki la P Square ameachiliwa kutoka gereza la Ikoyi baada ya muda wa miezi miwili.

Jude ambaye aliwahi kuwa meneja wa P Square, alikamatwa Februari 26, 2025 kufuatia uchunguzi uliotekelezwa na tume ya makosa ya kiuchumi na kifedha EFCC ambao ulimhusisha na madai ya utakatishaji wa Naira bilioni 1.38 pesa za Nigeria.

Ilidaiwa kwamba Jude kupitia kwa kampuni yake ya muziki Northside Music Limited alijipatia kwa njia isiyofaa dola milioni moja na pauni 34,537.59.

Wakati alifikishwa mahakamani Machi 3, 2025, Jude alikanusha mashtaka yote dhidi yake na kuachiliwa kwa dhamana ya Naira Milioni 100.

Paul Okoye aliwahi kuandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba kulikuwa na juhudi za kuhujumu kuachiliwa huru kwa kakake mkubwa lakini jana Jumatano jioni, alichapisha video zilizoonyesha Jude akiondoka korokoroni na akiungana tena na familia yake.

Hii ni baada yake kutimiza masharti yote ya dhamana.

Kwenye mojawapo ya video, watoto wa Jude wanaonekana wenye furaha kumwona baada ya muda huku wakimrukia na hata kusababisha aanguke chini huku wakikumbatiana.

Peter Okoye mmoja wa wanamuziki wa P Square ndiye chanzo cha masaibu ya kakake mkubwa Jude aliyemshtaki kwa EFCC kufuatia madai kwamba aligundua kampuni tofauti kuliko ile yao asilia ya Northside Entertainment.

Kulingana na Peter, Jude alikuwa amesajili kampuni nyingine kwa jina Northside Music na mapato yao ya muziki yalikuwa yameelekezwa kwenye akaunti za kampuni hiyo.

Website |  + posts
Share This Article