Diamond atoa mchango kwa hospitali ya BMH Dodoma

fedha hizo zinalenga kurahisishia mzigo wa kifedha watoto wenye ugonjwa wa Selimundu na upandikizaji Figo kwa Wananchi wenye mahitaji

Marion Bosire
2 Min Read

Naseeb Abdul Juma ambaye ni msanii wa muziki nchini Tanzania maarufu kama Diamond Platnumz jana alizuru Hospitali ya Rufani ya Benjamin Mkapa, BMH jijini Dodoma ambapo alitoa mchango.

Diamond na washirika wake, waliipa taasisi hiyo ya Afya shilingi Milioni 185 pesa za Tanzania ambazo zitatumika kusaidia katika matibabu ya kupandikiza uloto kwa Watoto wenye ugonjwa wa Selimundu na upandikizaji Figo kwa Wananchi wenye mahitaji.

Msanii huyo alisema kwamba hatua hiyo ya kuchangia kiasi hiko cha fedha ni mwanzo tu wa ushirikiano na taasisi ya BMH akiahidi atakuwa balozi wa kutangaza uwekezaji mkubwa uliofanyika katika BMH.

Aliongeza kusema kwamba atawashirikisha wadau wake wa katika kazi za sanaa na kampuni za kibiashara katika kuunga mkono kuchangia huduma za Afya hospitalini BMH.

“Niipongeze Serikali chini ya Uongozi wa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa hapa BMH, pia watumishi wa BMH kwa moyo wa kujitoa, wito na kuhudumia wananchi,” alisema Diamond.

Msanii huyo alifurahia kwamba huduma hizo za matibabu, awali zilikuwa zikipatikana nje ya nchi na sasa zinatolewa BMH.

“Watu wa mataifa ya nje ya Tanzania wanakuja kuzifuata Tanzania katika Hospitali ya BMH kama upandikizaji uloto, upandikizaji figo, upasuaji moyo na huduma nyingine nyingi” aliongeza Diamond alipotoa hutuba hospitalini humo.

Share This Article