Mwanamuziki wa Uganda Cindy Sanyu amefichua jambo ambalo ataangazia wakati ambapo atastaafu kutoka kwa kazi ya kutumbuiza jukwaani.
Rais huyo wa muungano wa wanamuziki wa Uganda UMA, alikuwa akizungumza kwenye mahojiano ambapo alifichua kwamba kustaafu kutoka jukwaani hakumaanishi atang’atuka kabisa kutoka tasnia ya muziki.
Cindy alisema mustakabali wa tasnia hiyo ni muhimu na anapanga kusalia humo na kusaidia wasanii chipukizi kwa kuwapa ushauri akisisitiza kwamba amejitolea kwa tasnia hiyo maisha yake yote.
“Maisha baada ya kutumbuiza kwangu yanamaanisha kubadili na kuingilia ushauri kwa wasanii na wala sio kuondokea tasnia ya muziki kabiisa” alisema Sanyu.
Katika mahojiano hayo Cindy alikumbuka jinsi aliingilia muziki akiwa na umri mdogo akifichua kwamba alianza kuandika nyimbo zake akiwa na umri wa miaka saba pekee.
Mamake alimuunga mkono huku akimtabiria kwamba siku moja atakuwa nyota mkubwa wa muziki akimlinganisha na Whitney Houston na Yvonne Chaka Chaka.
