Raia sita wa Iran waliokamatwa katika bandari ya Kilindini wakisafirisha mihadarati ya thamani ya shilingi bilioni 8.2, watazuiliwa kwa siku 30, ili kuwaruhusu polisi kukamilisha uchunguzi.
Hakimu wa mahakama ya Shanzu Anthony Muchigi, aliagiza washukiwa hao wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Port, huku maagizo zaidi yakisubiriwa.
Mahakama hiyo iliwaagiza maafisa wanaochunguza kesi hiyo, kuwasilisha mihadarati hiyo kwa maabara ya serikali na pia kuwasilisha simu za washukiwa hao katika Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa uchunguzi wa kisayansi.
Mahakama iyo ilifahamishwa kuwa washukiwa hao walikamatwa Oktoba 24,2025 na maafisa wa jeshi la wanamaji katika bandari ya Kilindini wakiwa kwenye mashua nyeusi.
Wakati wa kukamatwa kwao washukiwa hao walipatikana na kilo 1,035.986 za mihadarati.
Kesi dhidi yao itatajwa Novemba 14,2025.
