Maafisa wa polisi nchini Brazil wamesema kwamba walizuia shambulizi la bomu lililokuwa likipangwa dhidi ya tamasha la mwanamuziki wa Marekani Lady Gaga katika ufuo wa Copacabana huko Rio de Janeiro Jumamosi.
Polisi wa jimbo la Rio de Janeirokwa ushirikiano na wizara ya haki wanasema kwamba washukiwa walikuwa wamesajili wahudhuriaji fulani wa tamasha hilo watekeleze shambulizi hilo kwa kutumia vilipuzi vya kujitengenezea.
Lengo lao kuu lilikuwa kujipatia sifa mitandaoni.
Kulingana na polisi mhusika mkuu wa kupanga shambulizi hilo pamoja na kijana mmoja walikamatwa.
Kundi la Lady Gaga lilisema lilifahamu kuhusu shambulio hilo lililopangwa kutokana na ripoti za mitandao ya kijamii Jumapili asubuhi baada ya tamasha lao.
Umati wa watu wapatao milioni mbili ulikusanyika kwa ajili ya tamasha hilo ambalo halikuwa na ada ya kiingilio huku polisi wakisema wahusika wa shambulio hilo walieneza semi za chuki dhidi ya watoto, vijana wanaobaleghe na mashoga.
Mhusika mkuu alikamatwa kwa kosa la kumiliki bunduki kinyume cha sheria katika jimbo hilo la kusini la Rio Grande do Sul, huku kijana akikamatwa kwa kuwa na picha za ngono za watoto huko Rio.
Wapangaji hao wa shambulizi hilo wanadaiwa pia kupendekeza itikadi kali kwa vijana, waliwahimiza wajidhuru na kuwahimiza wachapishe maudhui ya vurugu ndiposa watambuliwe kama wanachama.