Mahakama Kuu imesimamisha kwa muda hatua ya kutimuliwa kwa Seneta mteule Gloria Orwoba kutoka chama cha UDA.
Katika agizo lake alilotoa leo Mei 21, 2025, Jaji Lawrence Mugambi alisema kwamba alisoma ombi lililowasilishwa na Orwoba chini ya hati ya dharura kabla ya kuagiza kusimamishwa kwa hatua hiyo hadi kesi yake itakaposikilizwa na kuamuliwa.
“Ninaelekeza kusimamishwa kwa utekelezaji wa uamuzi wa kamati ya nidhamu ya chama cha UDA wa Mei 19, 2025 wa kumtimua mwasilishaji wa ombi hili kama mwanachama na Seneta Mteule” alisema Jaji Mugambi katika agizo lake.
Jaji Mugambi amesema kwamba atatoa maelekezo zaidi kuhusu kesi hiyo Juni 3, 2025.
Katika mkutano wake wa Mei 19, 2025, kamati hiyo ya nidhamu ya chama cha UDA iliamua kwamba Orwoba atimuliwe kutoka kwa chama hicho kama mwanachama na hivyo kukomesha fadhila zote ikiwemo uteuzi kama Seneta.
Orwoba analaumiwa kwa kukiuka maadili ya chama cha UDA na kwa kukosa kufika mbele ya kamati hiyo ya nidhamu.
Katibu mkuu wa UDA Hassan Omar alisema siku hiyo kwamba walikuwa wamemwandikia Spika wa seneti waraka wa kumfahamisha kuhusu hatua hiyo na tayari Spika Amason Kingi ametangaza wadhifa huo kuwa wazi.
Chama cha UDA kimependekeza Consolata Wabwire Wakwabubi wa kaunti ya Bungoma kuchukua wadhifa wa Orwoba katika bunge la Seneti lakini mchakato huo umesimamishwa na mahakama.