Diamond asema amemwachilia Lava Lava bila malipo

Ameahidi pia kumpa ufadhili wa kuanzia kazi zake kama msanii huru.

Marion Bosire
1 Min Read
Lava Lava

Msanii wa muziki nchini Tanzania na mmiliki wa kampuni ya WCB Diamond Platnumz amefafanua kwamba alimwachilia msanii Lava lava aondoke kwenye kampuni hiyo bila malipo yoyote.

Akizungumza na wanahabari leo katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, Diamond alisema kwamba yeye ndiye alimpigia simu jamaa kwa jina Kim akamwambia iwapo Lava Lava angependa kuondoka aende kwake ampe uhuru wa kuondoka.

Kulingana naye mikataba sio kitu kikubwa inaweza kukiukwa kwa makubaliano isipokuwa kwa wasanii ambao huenda wakapungukiwa kimaadili.

Alitetea kampuni ya WCB kutokana na kile alichokitaja kuwa mtazamo wa umma kwamba haimsaidii Lava Lava katika kuinuka kama msanii akisema kwamba huenda mafanikio yake yako nje ya WCB.

Diamond Platnumz alisema pia kwamba alimahidi Lava Lava kwamba atampa hela ambazo zitamwezesha kuanza kazi kama msanii huru akimtaja kuwa ndugu yake ambaye anampenda sana.

Lava Lava ambaye jina lake halisi ni Abdul Juma Mangala, ndiye msanii wa hivi punde zaidi kuondoka WCB baada ya Mbosso kuondoka mwezi februari mwaka huu naye pia hakutakiwa kulipa chochote.

Wakati wa kutangaza kuondoka kwa Mbosso, Diamond alisema kwamba kampuni yake ya WCB itasajili wasanii wengine wapya mwaka huu wa 2025.

Website |  + posts
Share This Article