Chris Brown aachiliwa kwa dhamana

Ameachiliwa kwa dhamana ya Yuro milioni 5 na atarejea mahakamani Juni 20, 2025.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki kutoka Marekani Chris Brown ameachiliwa kwa dhamana ya Yuro milioni 5 na mahakama moja jijini London nchini Uingereza.

Ijumaa Mei 16, 2025 mahakama hiyo kupitia jaji Joanne Hirst, ilimnyima dhamana msanii huyo na angesalia rumande hadi Juni 13, 2025 wakati wa kurejeshwa mahakamani.

Kesi inayomkabili Brown ni ya kusababishia mtayarishaji wa muziki kwa jina Abe Diaw madhara mwilini, kisa kilichotokea mwaka 2023.

Februari 19, 2023, Brown alimshambulia Diaw ndani ya klabu cha burudani katika wilaya ya Mayfair wakati wa majibizano kati yao akitumia chupa ya pombe ambayo alimgonga nayo kichwani.

Msanii huyo sasa anaweza kuendelea na maandalizi ya ziara yake ya kikazi ya ulimwengu kwa jina “Breezy Bowl XX” inayostahili kuanza mwezi ujao.

Inaanza rasmi Juni 8, huko Amsterdam kabla ya kuelekea maeneo ya Manchester, London, Cardiff, Birmingham na Glasgow mwezi Juni.

Alikamatwa Mei 15, 2025 katika hoteli ya Lowry iliyoko Manchester na kufikishwa mahakamani kesho yake.

Brown wa umri wa miaka 36 hakuwa katika mahakama ya Southwark Crown leo Jumatano wakati wa kusikilizwa kwa ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana.

Dhamana hiyo ya Yuro milioni 5 ilitajwa na mahakama kuwa ada ya usalama. Ada ya usalama hutolewa kama njia ya kuhakikisha kwamba mshtakiwa anarejea mahakamani. Anaweza akapoteza pesa hizo iwapo atakiuka masharti ya dhamana.

Anahitajika kutoa Yuro milioni 4 kabla ya kuondoka rumande na milioni moja iliyosalia katika muda wa siku saba zijazo.

Juni 20, 2025 ndiyo siku anatarajiwa kurejea mahakamani.

Website |  + posts
Share This Article