Mwanamuziki wa kike wa Uganda Juliana Kanyomozi amesifia kazi ya Bebe Cool ambayo inatarajiwa kuzinduliwa Mei 30, 2025.
Juliana ni mmoja wa wasanii ambao Bebe Cool alialika kwa kikao cha kusikiliza nyimbo zilizo kwenye albamu yake kwa jina “Break The Chains” atakayozindua karibuni.
Kwa maoni yake Juliana alisema kazi ambayo mwanamuziki mwenza ameandaa ni ya kipekee huku akisifia ukuaji wake na uwezo wake wa kuimba mitindo tofauti.
Katika albamu hiyo Bebe Cool amechanganya mtindo wake wa kawaida na mtindo unaopendwa ulimwenguni kote wa Afrobeats huku akisimulia hadithi tofauti.
Juliana alielezea kwamba albamu hiyo inaunganisha ladha tofauti za muziki kwa kila mmoja akisema Bebe Cool anasikika tofauti katika kila wimbo ulioko.
Mwezi uliopita Bebe Cool alisema kwenye TikTok kwamba albamu hiyo itazinduliwa rasmi Ijumaa Mei 30, 2025 na kukomesha wasiwasi wa mashabiki zake ambao wamekuwa wakisubiri kwa hamu.
Tayari Bebe Cool amezindua vibao viwili ‘Circumference’ na ‘Motivation’ ambavyo viko kwenye albamu hiyo.
Albamu ya Break The Chains inatarajiwa kuonyesha mchanganyiko wa mtindo asilia wa Bebe Cool na mtindo maarufu wa sikuhizi wa Afrobeats pamoja na simulizi za hadithi.
Cool alisema uamuzi wake wa kuhusisha mtindo wa Afrobeats ulichochewa na mitindo ya sasa ya muziki ulimwenguni ambapo wasanii wengi wanaingilia mtindo wa Afrobeat.
Jina la ‘Break The Chains’ kulingana naye ni la kuashiria jinsi ya kukiuka vikwazo na kujisukuma zaidi na kupita dari ya kioo ambayo kwa miaka mingi imechukuliwa kuwa kikwazo kikuu kwa wasanii wa Uganda kuafikia ulimwengu mzima na kazi zao.
Bebe Cool anaamini kwamba albamu yake mpya itasaidia pakubwa kusukuma muziki wa Uganda hadi katika jukwaa la kimataifa.
Ameshirikisha watayarishaji muziki wapya, wahandisi na wengine katika maandalizi ya albamu hiyo.