Filamu kuhusu sokwe wa Rwanda yawekwa kwenye Netflix

Inasimulia kuhusu sokwe wa milimani wa Rwanda na miongo ya juhudi za uhifadhi kwa hadhira ya kimataifa.

Marion Bosire
2 Min Read

Filamu mpya ya hali halisi kuhusu utunzaji wa Sokwe wa Rwanda iliyopatiwa jina la “A Gorilla Story” imeanza kuonyeshwa kwenye jukwaa la kimataifa la filamu la Netflix.

Kazi hiyo ambayo msimulizi wake ni mwanahistoria wa asili wa Uingereza David Attenborough, imeonyeshwa kwa mara ya kwanza duniani kote ikisimulia kuhusu sokwe wa milimani wa Rwanda na miongo ya juhudi za uhifadhi kwa hadhira ya kimataifa.

Filamu hiyo inafuatilia maisha na ukoo wa familia ya sokwe wa Pablo, ikitoa mwonekano wa nadra na wa karibu kuhusu tabia za spishi hiyo na mifumo yake tata ya kijamii.

Attenborough, ambaye uhusiano wake na sokwe wa Rwanda ulianza tangu ziara yake ya mwaka 1978 katika Hifadhi ya Taifa ya Volcanoes, anachangia mtindo wake wa kipekee wa usimulizi katika mradi huu.

Filamu hiyo imetayarishwa na Silverback Films kwa ushirikiano na Appian Way Productions  iliyoanzishwa na Leonardo DiCaprio pamoja na Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB) na Dian Fossey Gorilla Fund.

Ilirekodiwa kwa kipindi kirefu katika Hifadhi ya Taifa ya Volcanoes, ikinanasa matukio ya karibu ndani ya makundi ya sokwe, ikifichua uhusiano wa vizazi na mienendo ya kuishi katika mojawapo ya mifumo ikolojia iliyolindwa kwa uangalifu zaidi duniani.

Zaidi ya picha zake za kuvutia, filamu hiyo inaangazia mfano wa uhifadhi wa Rwanda, ambao umechangia kuongezeka kwa idadi ya sokwe wa milimani katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.

Maafisa wanasema filamu hiyo haionyeshi tu wanyamapori bali pia inasimulia hadithi pana ya utunzaji endelevu wa mazingira.

Afisa Mkuu wa Utalii wa RDB, Irène Murerwa, alisema kazi hiyo inatoa jukwaa la kuwasilisha maendeleo ya kisayansi na juhudi za kibinadamu zilizo nyuma ya uhifadhi.

Share This Article