Pascal Tokodi msanii kutoka Kenya anaendelea kung’aa kama jaji mgeni katika shindano la uimbaji la Bongo Star Search, BSS msimu wa 16, lililoanza mwezi Machi mwaka huu.
Msimu huu kauli mbiu ya mashindano hayo ni “Mapinduzi ya Kiwango Kijacho/Zaidi ya Mipaka” na yameshirikisha washindani kutoka nje ya Tanzania hususan kutoka Kenya.
Majaji wenzake katika mashindano hayo ya uimbaji walimkaribisha Tokodi kwa moyo mkunjufu huku wakimtaja kuwa kiungo muhimu katka kazi yao.
Kwenye video fupi iliyochapishwa kwenye akaunti rasmi za Bongo Star Search majaji hao wakiwemo Rita Paulsen, Salama Jabir na Master Jay wanasikika wakitoa maoni yao.
Salama anasema kwamba, “Kuwa naye kwenye meza ni jambo la kujivunia, sana sana kwangu kwa sababu amewekwa karibu na mimi. Ninaweza kumkanyaga mguu, akikanyaga huku mimi nakanyaga huku.”
Master Jay kwa upande wake anasema kwamba Tokodi ana weledi katika nyanja tofauti za usanii kwani ni mwimbaji, mchekeshaji na mwigzaji kwa hivyo ni kama kuua ndege watatu kwa jiwe moja.
Rita Paulsen ambaye ni mwandalizi na jaji mkuu wa mashindano hayo alimsifia Tokodi akisema kwamba ana uwepo mzuri na alijua akijumuishwa na majaj wengine, watapatana.
Tokodi kwenye video hiyo anasema alipopigiwa simu kuhusu kujumuishwa kama jaji kwenye awamu ya 16, alifurahia sana, furaha iliyoongezeka alipogundua kwamba wataendesha mashindano katika hoteli ya Hilton.
Alisimulia kwamba kazi yake ya uimbaji ilianzia huko huko Hilton ambapo alijaribiwa kwenye shindano sawia kabla ya kuelekea Nigeria kwa fainali ya mashindano hayo ambapo aliibuka mshindi.
Mashindano ya Bongo Star Search huonyeshwa kila Jumapili saa mbili usiku huku video za matukio ya mashindano hayo zikionyeshwa Ijumaa na Jumapili kwenye Azam Tv, Sinema Zetu.