Msanii tajika wa muziki kutoka Nigeria Davido alishindwa kuzuia machozi alipokuwa akitoa hotuba katika hafla ya ndoa ya kitamaduni ya meneja wake aitwaye Asa Asika.
Davido alikuwa akizungumzia safari yao ya miaka 14, ambapo alikumbuka jinsi watu wengine walikosa imani kwamba angefika alipofikia leo, kabla ya kuanza kulia na kushindwa kuzungumza.
Ilibidi aketi karibu na Asa na mkewe ambao walionekana wakimpapasa kama njia ya kumtia moyo na akasimama na kuendelea kuhutubu.
Baadaye kupitia Instagram Davido aliandika, “Siku ya leo imenivunja Leo imenivunja… kwa njia ya kupendeza zaidi. Kukuona ukiwa umesimama kando ya Leona, ukiwa na amani machoni na upendo moyoni – singeweza kujizuia.”
Davido aliendelea kumsifia meneja wake kwa hatua ambazo amepiga maishani na alikopitia kabla ya kufika aliko akisema, “Hakuna tulichopatiwa bure. Tulijijenga – kupitia moto, kupitia imani na uhusiano ambao haukuwahi kuvunjika.”
Alisema kando na kuwa meneja wake, Asa alikuwa pia ngao yake, alihakikisha hali nzuri ya akili yake, akawa ndugu yake katika kila pambano, alikwama naye kila kulipoharibika jambo na hata sasa ambapo wameafikia mengi amesalia kuwa yule yule aliyeanza naye.
Mwanamuziki huyo alimtania meneja wake akisema kwamba tangu alipoanza uhusiano na Leona amekuwa laini, anatabasamu zaidi na ana amani.
Alimshukuru Leona kwa kumpenda Asa akisema kwamba amejiunga na safari na sasa yeye ni kusudi la safari hiyo.