Sheila Carol Gachumba ambaye wengi wanamfahamu tu kama Sheila Gashumba, ameahidi kugharamia kikamilfu masomo ya msichana raia wa Uganda aliyeonekana akitumia usafiri wa baiskeli kuelekea shuleni.
Gashumba ambaye ni mtangazaji maarufu nchini Uganda aliguswa na video ya msichana huyo kwa jina Blessing Angel Atuhaire iliyosambaa mitandaoni inayomwonyesha akiendesha baiskeli akiwa amevaa sare kamili ya shule, mkoba mgongoni huku mvua ikinyesha.
Video hiyo iligusa wengi nchini Uganda na kusababisha wengi wamwonee binti huyo huruma na kuhimiza apate usaidizi stahiki kwa kujitolea kwake kwa masomo.
Gashumba ameahidi kumlipia msichana huyo karo ya shule hadi kiwango chochote cha masomo anachotaka kufikia, kupitia mpango wake wa udhamini wa masomo chini ya wakfu wake Sheilah Gashumba Foundation.
Mwanahabari aitwaye Gideon Nova Kwikiriza amekuwa akishiriksha juhudi za kusaidia msichana huyo kwenye mtandao wa X ambapo Gashumba aliweka maoni yake akimwambia, “Nijuze utakapompata msichana huyo. Anaonekana kujitolea kwa elimu yake, kuendesha baiskeli kwenye mvua!”
Gashumba aliendelea akisema, “Abarikiwe. Niko tayari kulipa karo yake katika shule ya bweni hadi akamilishe masomo yake.”
Kwirikiza aljibu akisema amewasiliana na waliorekodi video hiyo ambao ni Bakiga Tv na ana imani kwamba watamsaidia kufikia msichana husika ili asaidiwe.