Rais William Ruto kwa mara nyingine ametetea ushirikiano uliopo kati ya chama tawala Kenya Kwanza na chama cha upinzani ODM.
Akizungumza huko Suna Mashariki jana katika ibada ya madhehebu mbali mbali, Rais Ruto alisema kwamba makubaliano kati ya Kenya Kwanza na ODM yanalenga ushirikiano na wala sio ushindani wa kisiasa.
Ruto alisema kwamba kujitolea kwake katika makubaliano na kiongozi wa ODM Raila Odinga kulichochewa na haja ya kuhakikisha mazuri kwa wakenya wote badala ya maazimio ya kibinafsi.
Rais alisisitiza kwamba umoja wa kitaifa una thamani kubwa sana kuliko ushindi wa kibinafsi katika siasa.
Wakati huo huo kiongozi wa nchi aliwataka viongozi wa pande zote za siasa kuweka kando tofauti zao na kutoa kipaumbele kwa utoaji huduma kwa wananchi.
Viongozi waliochaguliwa wa kaunti ya Migori waliokuwepo walimkaribisha Rais Ruto wakiahidi kushirikiana na serikali ya kitaifa kusuluhisha changamoto mbali mbali za eneo hilo.
Rais Ruto yuko katika eneo hilo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo anatarajiwa kuzindua miradi ya maendeleo na kukagua mingine inayoendelea ukiwemo mradi wa nyumba za bei nafuu.