Waziri wa Kilimo na Ustawishaji wa Mifugo Mutahi Kagwe ameamrisha kuharibiwa kwa magunia 27,518 ya mbolea iliyopita muda wake wa matumizi, inayohifadhiwa katika ghala za Halmashauri ya Nafaka na Mazao (NCPB) kote nchini.
Shirika la Ukadiriaji Ubora wa Bidhaa nchini (KEBS) litasimamia zoezi la kuharibu shehena hiyo ya mbolea aina ya Sulphate of Ammonia, iliyowasilishwa katika ghala za NCPB na kampuni ya Fine Tech Edge kati ya Disemba 27 mwaka 2024 na Januari 6 mwaka huu.
Mbolea hiyo ilikuwa imetimiza viwango vya ubora vinavyohitajika kwa matumizi kabla ya kutolewa kwa zabuni ya usambasaji kulingana na tathmini iliyofanywa na KEBS.
KEBS iliidhinisha magunia 34,100 ya kilo 50 kila moja kuwasilishwa kwa NCPB na kampuni iliyopewa zabuni, lakini baadaye ikaonekana kuwa muda wake wa matumizi ulikuwa ukamilike tarehe 28 mwezi jana, ndiposa NCPB ikaagiza kusambazwa kwa shehena nyigine ya mbolea iliyo na muda mrefu wa matumizi.
Aidha, NCPB ilitoa agizo la kusitisha uuzaji wa mbolea hiyo Februari 27 na kuzuia usafirishaji wake tarehe 4 mwezi huu, hadi pale shehena ya mbolea iliyopita muda wa matumizi itakapoharibiwa.
Waziri Kagwe amekariri kujitolea kwa serikali kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo za hali ya juu kulingana na viwango vilivyowekwa.