Michelle Obama mke wa aliyekuwa Rais wa 44 wa Marekani Barack Obama na kakake mkubwa Craig Robinson wameazisha kipindi cha mitandaoni kitakachoangazia pakubwa maisha yao.
Kipindi hicho wamekipa jina la In My Opinion – IMO yaani ‘Kwa Maoni Yangu’ na kutakuwa na makala kila Jumatano.
Kando na maisha yao, watakuwa pia wakihoji wageni mbali mbali ambao wengi ni watu maarufu kama Issa Rae, Glennon Doyle, Jay Shetty, Dwyane Wade, Seth Rogen, Tracee Ellis Ross na Keke Palmer.
Michelle anaonekana kufuata nyayo za mume wake ambaye miaka minne iliyopita, alishirikiana na Bruce Springsteen na kuzindua kipindi cha mitandaoni kinachofahamika kama “Renegades: Born in the USA”.
Huku haya yakijiri, kuna jamaa watatu wanaoishi Uingereza wanaoaminika kuwa wa asili ya Nigeria ambao wamelalamikia hatua hii ya Michelle.
Kisa na sababu, amechukua jina la kipindi chao cha mitandaoni, In My Own Opinion.
Watatu hao DT, Uzoma na Mulinde walichapisha video wakilalamika kwamba wamekuwa wakichapisha maudhui mitandaoni kwa miaka mitano sasa chini ya jina hilo na hawataki kulipoteza.
Walimhimiza atafute jina jingine la kipindi chake wakisema kwamba hawataki ushawishi wake mkubwa uwafunike ilhali wamekuwa wakijitahidi kufika walipo.
Walipoulizwa iwapo wamesajili hakimiliki ya jina hilo watatu hao walisema wamesajili jina hilo nchini Uingereza pekee.
Inasubiriwa kuona iwapo video yao itamfikia Michelle Obama na majibu yake yatakuwa yapi.