Mwanamuziki wa Tanzania William Nicholaus Lyimo maarufu kama Billnass amekanusha madai ya kuwa sababu kuu ya mwanamuziki Yammi kuondoka kampuni ya muziki ya The African Princess.
Kampuni ya The African Princess inamilikiwa na mke wa Billnass, Nandy na uvumi ulisambaa mitandaoni kwamba Billnass alisababisha mkataba wa Yammi usitishwe.
Anadaiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Yammi madai aliyokanusha Nandy.
“Sijajua ni nani ambaye ameanzisha hizi habari za kunichafua mimi, yaani inabidi watu waniheshimu sana kwenye haya mambo, sina ujinga huo na wala sijawahi kufanya hivyo na yule binti tunaheshimiana sana,” alisema Billnass.
Aliendelea kusema kwamba wengi wanadhania kwamba mkewe Nandy anamtetea katika suala hilo lakini sio kweli kwani Nandy anaelewa kwamba ni uvumi unaolenga kuharibu ndoa yao na kuitia doa.
“Kwanza Yammi tunamfahamu mpenzi wake na wala hatuna shaka naye, ameondoka kwa uzuri hana mgogoro wowote na mke wangu wala mimi, ifike hatua watu tuheshimiane jamani” alisema Billnass.
Tarehe 5 mwezi huu wa Mei mwaka 2025 Nandy alitangaza rasmi kwamba mkataba kati ya kampuni yake na Yammi ulikuwa umehitimika baada ya majadiliano na makubaliano kati yao.
Nandy alimtakia Yammi kila la heri katika kazi zake za siku zijazo.