Aslay asisimua mashabiki Nakuru

Alikuwa mtumbuizaji mkuu katika tamasha ya Reunion 2.0 Jumamosi usiku mjini Nakuru.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Bongo Fleva kutoka Tanzania Aslay Isihaka Nassoro, maarufu kama Aslay, alisisimua mashabiki wake huko Nakuru, alipotumbuiza Jumamosi usiku katika tamasha ya Reunion 2.0.

Msanii huyo ambaye aliingilia muziki akiwa na umri wa miaka 15 pekee, aliwapa waliohudhuria tamasha hiyo vibao vyake pendwa kama Mhudumu na Naenda Kusema.

Alichapisha video fupi kwenye akaunti yake ya Instagram iliyoonyesha matukio ya tamasha hiyo alipokuwa akiingia jukwaani na alipokuwa akitumbuiza anapoendeleza ziara yake ya kikazi nchini Kenya.

Aslay alianza na wimbo wa mhudumu ambapo mara kwa mara, mpiga muziki alikuwa anazima rekodi na kuacha umati uliojaa msisimko, uimbe pamoja na msanii huyo.

Wimbo uliompa Aslay umaarufu ni “Naenda Kusema” aliotoa mwaka 2011 akiwa mchanga tu, wimbo unaogusia maadili ya kijamii ambapo baba anashtuliwa kwa kuwa na mahusiano nje ya ndoa.

Baada ya Nakuru, Aslay alitumbuiza tena jijini Eldoret usiku wa jana Mei 3, kabla ya kuja Nairobi Mei 8 na 9, 2026.

Msanii huyo ambaye sasa ana umri wa miaka 30, atatumbuiza pia nchini Saudi Arabia mwisho wa mwezi huu wa Mei na Agosti aandae tamasha mjini Goma nchini Congo kabla ya kuelekea Australia.

Alianza kazi kama mwanamuziki chini ya usimamizi wa kampuni ya Mkubwa na wanae ambayo ilibuni kundi la muziki la Yamoto Band mwaka 2013, kundi lililojumuisha Aslay, Mbosso na Enock Bella.

Sasa hivi Aslay anasimamiwa na kampuni ya Rockstar Africa pamoja na Sony Music Africa.

Share This Article