Msanii wa muziki nchini Marekani Sean ‘Diddy’ Combs ambaye amezuiliwa katika gereza la Brooklyn akisubiri kesi dhidi yake anaripotiwa kukimbizwa hospitalini kutoka gerezani humo.
Diddy wa umri wa miaka 55 anasubiri kesi yake inayohusiana na ulanguzi wa binadamu ili kuwatumia kingono isikilizwe mwezi Mei mwaka huu.
Alikamatwa Septemba 2024 hata ingawa amekanusha madai dhidi yake na amenyimwa dhamana mara kadhaa.
Mwanamuziki huyo anaripotiwa kukimbizwa kwenye hospitali moja huko Brooklyn kwa kile kilichotajwa kuwa vipimo baada ya kulalamikia maumivu kwenye goti.
Alilazwa kusubiri vipimo vya MRI ili kufahamu kinachomsibu.
Msemaji wa gereza anakozuiliwa alikataa kutoa habari zaidi akisema kwamba huwa hawatoi taarifa kuhusu wafungwa kwa sababu ya ulinzi na usalama wao.
Maafisa wa usalama wanaripotiwa kufahamishwa kuhusu hatua ya kumpeleka Diddy hospitalini iwapo ingefahamia kwamba yuko hospitalini na vurugu zizuke.
Baada ya kukamatwa mwaka jana kutokana na madai ya awali, Diddy amekuwa akikabiliwa na kesi nyingine kutoka kwa watu wanaodai kudhulumiwa naye kingono.
Hata hivyo anashikilia kwamba hakutenda kosa lolote na anasubiri kujiondolea lawama mahakamani tarehe 5 mwezi Mei wakati kesi dhidi yake itaanza kusikilizwa.