Rais William Ruto amepangiwa kuhutubia taifa leo Ijumaa asubuhi, siku moja baada ya kurejea nchini kutoka kwenye ziara za kitaifa katika mataifa ya bara Asia ya Azerbaijan na Kazakhstan.
Ruto, ambaye alianza ziara ya maendeleo ya siku tano eneo la Pwani jana Alhamisi, atahutubia taifa kutoka Ikulu ya Mombasa kuanzia majira ya saa mbili.
Rpoti zinaashiria alikutana na wadau wa magari ya uchukuzi wa umma ikuluni hapo jana kuzungumzia masaibu yanayowasonga.
Wadau hao walikubali kusitisha mgomo wa matatu kwa wiki moja ili kupisha mazungumzo na serikali kuhusiana na bei za juu za mafuta wanazosema zimeathiri mno utendaji kazi wao.
Wametishia kuitisha tena mgomo ikiwa serikali itafumbia macho malalamiko yao baada ya kukamilika kwa kipindi hicho cha siku saba.
Suala la bei za juu za mafuta linasemekana kuwa kiini cha mazungumzo kati ya Ruto na wadau hao wakati wa mkutano kati yao hapo jana.
Kwa misingi hiyo, wengi watasubiri kuona makubaliano ambayo yalifikiwa kupunguza bei za juu za mafuta ambazo yamkini zimeathiri kila sekta nchini.
Wadau wa sekta ya uchukuzi wa umma wanashinikiza kupunguzwa kwa bei ya mafuta kwa angalau shilingi 46 ili kurahisisha utendaji kazi wao.
Hata hivyo, serikali ilitangaza kupunguza bei ya dizeli kwa shilingi 10.06 kwa lita huku ikiongeza bei ya mafuta taa kwa shilingi 38.60 kwa lita.
Ni punguzo ambalo wadau wametaja kuwa lisilotosheleza.