Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), wamewakamata wanawake wawili eneo la Nyando kaunti ya Kisumu kwa kosa la kumiliki bastola kinyume cha sheria.
Sharon Auma na Nancy Atieno Obura walitiwa nguvuni baada ya kushikwa wakiwa na bastola aina ya Canik, iliyokuwa imefichwa chini ya kitanda.
Kulinga na DCI kupitia ukurasa wa X, wawili hao walikamatwa baada maafisa hao wa usalama kupashwa habari kuhusu sharon Auma aliyekuwa ameweka picha yake akiwa na bastola kwenye mtandao wa WhatsApp, akitishia kuwa mwananume yeyote atakayemuacha, atakina cha mtema kuni.
Maafisa wa polisi walichukua hatua za haraka na kumkamata Sharon mjini Awasi. Baada ya kumhoji, aliwapeleka maafisa hao kwenye nyumba ya rafiki yake Nancy Atieno Obura ambaye sasa ni mshtakiwa mwenza ambako bastola hiyo ilipatikana imefichwa mvunguni mwa kitanda.
Aidha maafisa hao pia walipata nambari bandia ya usajili wa pikipiki KMGG 805M.
Washukiwa hao wawili wanahojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani, huku washukiwa zaidi wakiendelea kusakwa kuhusiana na bastola hiyo.