Vikosi vya RSF vimetangaza serikali mbadala nchini Sudan

Tom Mathinji and BBC
2 Min Read
Kiongozi wa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF), Mohamed Hamdan "Hemedti" Dagalo.

Vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan, vimetangaza kuundwa kwa serikali mbadala, huku vita nchini humo vikiingia mwaka wa pili.

Tangazo hilo limejiri wakati ambapo mkutano umeandaliwa Jijini London kuadhimisha mwaka wa pili tangu mzozo ulipoanza nchini Sudan.  Katika mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy alitoa wito wa kupatikana kwa “amani”.

Kiongozi wa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF), Mohamed Hamdan “Hemedti” Dagalo, alisema kundi hilo “limeunda mustakabali wa kweli wa Sudan”.

Mapigano yaliendelea, huku jeshi likisema lilikuwa limeshambulia kwa mabomu vituo vya RSF nje ya mji wa el-Fasher, na kulazimisha mamia kwa maelfu kukimbia kambi ya wakimbizi ya Zamzam.

Hemedti alisema RSF inajenga “taifa lenye sheria” na sio dola inayotawaliwa na watu binafsi.

“Hatutafuti utawala bali umoja. Tunaamini kwamba hakuna kabila, eneo au dini inayoshikilia utambulisho wa Sudan,” taarifa yake kwenye Telegram ilisoma.

Aliongeza kuwa serikali yake itatoa huduma muhimu kama vile elimu na afya kwa sio tu maeneo yanayodhibitiwa na RSF, lakini nchi nzima.

Zaidi ya watu 400 wameuawa katika mashambulizi ya hivi majuzi ya RSF, kulingana na Umoja wa Mataifa, ikitoa “vyanzo vya kuaminika”.

Miaka miwili ya vita, jeshi na RSF wameshutumiwa kwa uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji ya halaiki na unyanyasaji mkubwa wa kingono.

Hemedti amekuwa katika mzozo wa kung’ang’ania madaraka na mkuu wa jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, tangu Aprili 15, 2023, na kusababisha mzozo wa kibinadamu ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 150,000 huku zaidi ya watu milioni 12 wakikimbia makazi yao.

Mashirika ya kibinadamu yameripoti hali kama njaa inayowakabili zaidi ya watu 700,000 katika kambi za muda karibu na El-Fasher, huku vitisho vya usalama na vizuizi vya barabarani vikizuia utoaji wa misaada muhimu.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article