Baadhi ya wazee katika kaunti ya Garissa, wametoa wito kwa asasi za usalama kuimarisha vita dhidi ya matumizi ya mihadarati mjini Garissa na viunga vyake.
Wakiongozwa na kundi la viongozi wa kiislamu (NAMLEF), wazee hao walisema kuwa utumizi wa dawa za kulevya mjini Garissa umeongezeka katika kiwango cha kutia wasiwasi.
Wakiwahutubia wanahabari katika hoteli moja mjini Garissa, wazee hao walidokeza kuwa tatizo hilo haliwezi achiwa serikali pekee kukabiliana nalo, mbali wananchi pia wanajukumu la kutekeleza la kutoa habari kwa asasi husika kuhusu walanguzi na watumizi wa mihadarati.
Mweka hazina wa NAMLEF Mohamed Hassan, alisema kuwa baadhi ya mihadarati huuzwa hadharani na kusababisha ongezeko la visa vya wizi nyakati za mchana pamoja na aina zingine za uhalifu katika eneo hilo.
“Lazima tuangamize ulanguzi huu. Hii ndio njia pekee ya kupiga hatua dhidi ya utumizi wa dawa za kulevya ambao umeghubika eneo hili,” alisema Hassan.
Kulingana na Shirika la kukabiliana na utumizi wa mihadarati nchini NACADA, miraa, bangi na cocaine, ni miongoni mwa dawa za kulevya zinazotumia zaidi katika kaunti ya Garissa.
“Ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa, ulanguzi na utumizi wa mihadarati katika eneo hili utashindwa kudhibitiwa na kusababisha ukosefu wa usalama katika eneo hili,” aliongeza Hassan.
Aidha wazee hao waliwalaumu viongozi wa eneo hilo kwa kusalia kimya huku matumizi ya mihadarati yakiendelea kuongezeka.