Mwanamke mmoja mkazi wa jimbo la Texas nchini Marekani na mume wake wamekiri mashtaka ya kuchora watoto wawili tatoo nyumbani kwa kutumia pini na kuwatoa nyama mwilini katika harakati hizo.
Alhamisi iliyopita, Megan Farr wa umri wa miaka 29, alikubali mashtaka dhidi yake ya kufunga watoto hao na mashtaka manne ya kuwasababishia majeraha kimakusudi.
Kulingana na maafisa wa polisi, wakati baba mzazi wa watoto hao alimkaripia Megan, alikiri kufanya hivyo na akacheka.
Taarifa ya polisi inaashiria kwamba watoto hao walionekana kana kwamba walinyofolewa nyama baada ya kufungwa kwa kamba, kufungwa macho na kufungwa midomo wasije wakapiga kelele.
Megan alifikishwa mahakamani baada ya mume wake Gunnar Farr ambaye ni baba wa kambo wa watoto hao wa umri wa miaka 25 kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani kwa shtaka la kufunga watoto hao, na miaka mitano kwa kila kosa la kuwasababishia majeraha.
Vifungo hivyo vitaendelea kwa wakati mmoja huku Megan akitarajiwa kuhukumiwa baadaye.
Wanandoa hao walikamatwa Aprili 24, 2023, kufuatia uchunguzi uliotekelezwa na afisi ya huduma za utunzaji wa watoto na afisi ya mkuu wa polisi katika eneo la Angelina huko Texas.
Kulingana na taarifa rasmi za kukamatwa kwao wawili hao waliwafunga watoto hao ambao walikuwa wa umri wa miaka 9 na 5 kwa kamba, wakawafunga midomo kwa kutumia mkanda, wakawafunga macho kwa vitambara kabla ya kuwapa michoro hiyo.
Mmoja alichorwa kwenye mguu na mwingine akachorwa kwenye bega na wakati wa tukio hilo, marafiki wa wanandoa hao walikuwepo.
Baada ya hapo, wanandoa hao walijaribu kufuta michoro hiyo kwa kukata watoto hao, kuwakwaruza na kuwafuta kwa kutumia maji ya limau.