Uchunguzi wa maiti ya Albert Ojwang’ ulitekelezwa mchana wa leo na ulibainisha kwamba alishambuliwa kwani mwili huo una majeraha mbali mbali.
Ojwang’ alifariki katika mazingira ya kutatanisha katika kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi, aiku moja tu baada ya kukamatwa huko Homa Bay na kusafirishwa hadi Nairobi.
Bernard Midia ambaye ni mwanapatholojia wa serikali ndiye alitekeleza uchunguzi wa maiti ya Ojwang’ leo na kulingana naye, Ojwang’ hakujigongesha ukutani hadi akafariki kulingana na ripoti ya awali ya polisi.
Midia alisema walichunguza hali ya majeraha yaliyo kwenye mwili wa mwendazake hasa yale ya kichwa na kubaini kwamba hayakutokana na kujigongesha kwenye ukuta.
Kulingana naye iwapo majeraha hayo yangekuwa ya kujigongesha ukutani, yangekuwa na muundo sawa na uvujaji damu ungeshuhudiwa kwenye sehemu ya mbele ya kichwa cha mwendazake.
“Majeraja ya kuvuja damu tuliyoshuhudia kwenye ngozi ya kichwa chake yalikuwa na nafasi kati yao, yakiwemo ya usoni, kando kando ya kichwa na hata nyuma ya kichwa” alielezea Midia.
Midia alitekeleza uchunguzi huo mwakilishi wa familia ya marehemu kwa jina Mutuma Zambezi akiwepo na amekanusha uwezekano wa Ojwang’ kujisababishia majeraha.
Majibu ya uchunguzi wa leo yanakinzana na ripoti ya polisi iliyotolewa Jumapili iliyosema kwamba Ojwang’ alijigongesha kwenye ukuta wa seli katika kituo cha polisi cha Central.