Wasimamizi wa soka nchini watakiwa kuimarisha mchezo huo hadi viwango vya kimataifa

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais Ruto akabidhi timu ya taifa ya soka ya wachezaji chini ya miaka 20, bendera ya taifa.

Rais William Ruto amesema serikali inajizatiti kuimarisha miundombinu hapa nchini, ili kuwawezesha vijana kukuza talanta na vipaji vyao katika michezo.

“Lengo letu kuu ni kuinua kiwango cha mchezo wa soka katika ngazi za kimataifa, kama jinsi ilivyo katika riadha,” alisema Rais Ruto.

Akizungumza leo Jumanne katika Ikulu ya Nairobi alipokabidhi bendera kwa timu ya taifa ya soka kwa wachezaji walio na umri chini ya miaka 20 ambayo itashiriki katika michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika nchini Misri, kiongozi wa taifa alitoa changamoto kwa viongozi na wasimamizi wa soka hapa nchini kuinua hadhi ya mchezo huo hadi katika viwango vya kimataifa.

“Mna jukumu kuu la kuinua hadhi ya mchezo wa soka hapa nchini hadi katika viwango vya kimataifa sawia na ilivyo katika riadha,” alisema Rais Ruto.

Wasimamizi wa soka nchini, watakiwa kuimarisha mchezo huo hadi viwango vya kimataifa.

Kiongozi wa taifa aliongeza kuwa, ” Tunataka kuona Harambee Stars ikiinuka hadi kiwango cha Kimataifa. Ikizingatiwa kuwa wachezaji wengi wamechezea ligi za kimataifa, ni ishara tosha kuna talanta hapa nchini,”.

Kenya imewekwa katika kundi B pamoja na Nigeria, Morocco na Tunisia.

Michuano ya kuwania taifa bingwa Afrika kwa wachezaji walio na umri chini ya miaka 20 itaandaliwa kati ya Aprili 27 hadi Mei 18, 2025 nchini Misri.

Website |  + posts
Share This Article